KESHO HAIKUFIKA.
Mbunifu Cyphon
August 27, 2026
4 min read
186 views
1 favorites
Open Access
# SUMMARY OF THE WORK
Kesho Haikufika ni hadithi ya kubuni inayochunguza uhusiano kati ya upendo, afya, majuto na thamani ya muda. Inasimulia kuhusu kijana anayemtembelea mpenzi wake hospitalini akiwa katika hali mbaya ya kiafya baada ya kupuuza kwa muda mrefu ushauri wa kujitunza na kuacha sigara.
Katika mazungumzo yao, mgonjwa anafichua mipango ambayo walikuwa wakiiahirisha kwa kuamini kwamba bado wana muda—kuacha tabia hatarishi, kutunza afya, kujenga maisha yao na hatimaye kufunga ndoa. Lakini afya yake inapozidi kudhoofika, anagundua kwamba “kesho” si ahadi ambayo mwanadamu anaweza kuimiliki.
Baada ya kifo chake, msimulizi anakutana na orodha ya mambo ambayo mpenzi wake alipanga kufanya “kesho.” Tukio hilo linamfanya atafakari maisha yake mwenyewe na kuelewa kwamba afya, upendo, familia na muda ni vitu ambavyo mara nyingi tunavithamini baada ya kuanza kuvipoteza.
Hadithi hii inalenga kumfanya msomaji ajiulize: Ni mambo gani tunayoyaahirisha leo kwa sababu tunaamini tutakuwa na kesho?
KESHO HAIKUFIKA.
Siku ya mwisho kumuona akiwa hai, aliniuliza swali ambalo sikuwahi kudhani lingekuwa la mwisho.
“Ukinikumbuka, utanikumbuka kwa lipi?”
Nilicheka.
“Kwa tabia zako za kunikera.”
Akatabasamu.
“Basi usinisahau.”
Nilidhani tunataniana tu. Sikujua kama siku hiyo, chumba kile cha hospitali kilikuwa kikifunga sura ya maisha tuliyokuwa tukiyasogeza mbele kila siku.
Alikuwa amelala pale kitandani, amechoka kuliko nilivyowahi kumuona. Mrija wa drip ulikuwa ukining’inia pembeni, huku mashine ya mapigo ya moyo ikitoa sauti ndogo za taratibu.
Nilipoingia, alijaribu kutabasamu.
“Umechelewa.”
“Foleni ilikuwa ndefu.”
“Uongo.”
“Kwanini?”
“Maana wewe huwa unachelewa hata kusiwe na foleni.”
Nilicheka, naye akacheka. Kwa sekunde chache tu, chumba kile kikawaza kama sehemu ya kawaida kabisa.
Kisha akaniangalia vizuri.
“Unajua nilichogundua?”
“Nini?”
“Afya ni kitu cha ajabu sana.” Alitulia kidogo kabla ya kuendelea. “Ukiwa nayo, unaichukulia kama hewa tu. Unavuta na kuendelea na mambo yako. Lakini ikianza kuondoka, ndio unagundua ulikuwa umekalia utajiri mkubwa ambao hukuwahi hata kuuhesabu.”
Akimya kidogo.
“Nilikuwa naambiwa nipunguze sigara.”
“Aina hiyo nilijua.”
“Nilikuwa naambiwa nifanye mazoezi.”
“Nilijua pia.”
“Nilikuwa naambiwa nikiendelea kujisikia hivi niende hospitali.”
“Nilijua.”
Alinitazama.
“Na mimi nilikuwa nasema nini?”
Nilishusha macho. Alijijibu mwenyewe:
“Kesho.”
Neno hilo lilinichoma sana maana sote tulikuwa wachezaji wa mchezo huo:
Kesho tutaanza mazoezi.
Kesho tutaenda hospitali.
Kesho tutaacha sigara.
Kesho tutapanga maisha wetu.
Tulikuwa tumefanya 'kesho' kuwa jibu la kila kitu. Lakini siku hiyo ndipo nilipoanza kuelewa kuwa kesho ni ahadi ambayo maisha hayajawahi kuahidi kuitimiza.
“Nilikuwa mjinga sana,” alisema.
“Usiseme hivyo bwana.”
“Kwanini nisiseme? Ukweli haubadiliki kwa sababu tu tunauogopa.”
Aligeuza kichwa kutazama dirishani. Kutokea ghorofani pale, mji wa nje uliendelea na mambo yake kama kawaida. Magari yakipita, watu wakikimbizana na shughuli zao.
Akaonyesha chini kwa kidole.
“Unamwona yule?”
Nilitazama. Mwanaume mmoja alikuwa amesimama karibu na geti la hospitali, akivuta sigara taratibu.
“Eeh, namwona.”
“Nilikuwa kama yeye.” Akashusha breath. “Nilikuwa najiambia bado nina muda mwingi.”
Nilimtazama. “Na sasa hivi?”
Akaweka mkono kifuani. “Sasa hivi natamani tu ningeweza kurudisha siku nyuma.”
Macho yakaanza kumlengeta machozi.
“Daktari kasema sigara imechangia sana kuleta hii saratani ya mapafu. Nilikuwa najua madhara yake, lakini bado nikawa najiambia nitabadilika kesho.”
Akaangalia mikono yake ilivyokonda.
“Mbona nilikuwa na mipango mingi hivi...”
“Mipango gani?”
“Nilitaka tujenge nyumba...” Akatabasamu kwa uchungu. “...nilitaka tufunge na ndoa kabisa.”
Nilikausha, sikujua la kusema.
“Hukuniambia haya yote.”
“Nilikuwa nasubiri wakati sahihi.”
“Na sasa?”
Akanitazama moja kwa moja machoni. “Sasa nimeelewa kuwa wakati sahihi ni huu tulionao sasa hivi.”
Nilimshika mkono uliokuwa umeanza kupoteza joto. “Tutafanya yote ukipona.”
Akatabasamu kwa unyonge. “Usinipe ahadi ambayo kesho inaweza kuikataa.”
Kauli hiyo ilinikata kabisa.
Kabla sijamjibu kitu, ile mashine ya mapigo ya moyo ilianza kutoa mlio wa mfululizo na mkali. Madaktari na manesi wakaingia mbio chumbani.
“Mtoe nje kwanza!” Daktari mmoja alisukuma maneno kwa haraka.
Nilisimama huku miguu ikiwa haina nguvu. Mlango ukagongwa na kufungwa usoni kwangu.
Dakika moja.
Dakika mbili.
Tano.
Nilikuwa natazama ule mlango kama mtu anayesubiri hukumu.
Hatimaye daktari akatoka. Alinitazama, akavua baraghashia/kofia yake, kisha akainamisha kichwa. Hakuhitaji kusema kitu. Nilishatambua kilichotokea.
Usiku huo nilirudi nyumbani peke yangu.
Nilipofungua mlango wa chumba chetu, koti lake lilikuwa bado lipo kwenye kiti. Juu ya meza kulikuwa na pakiti ya sigara aliyokuwa ameahidi kuipiga chini. Pembeni yake kulikuwa na karatasi iliyokunjwa vibaya.
Niliifungua. Ilikuwa orodha ya mambo aliyotaka kufanya:
• Kuacha sigara.
• Kuanza mazoezi.
• Kusafiri.
• Kujenga nyumba.
• Kufunga ndoa.
• Kuanza maisha mapya.
Na chini kabisa alikuwa ameandika:
“Nitaanza kesho.”
Nilikaa chini sakafuni na kulia sana. Sikulia kwa sababu tu amefariki; nililia maana niligundua tulikuwa tunasubiri maisha yaanze siku zijazo, kumbe maisha yalikuwa yanapita hivi hivi tukiwa tunatazama.
Kesho yake nilirudi hospitali kuchukua vitu vyake.
Nilipopita kwenye ile korido na kusimama pale dirishani, nilitazama chini. Mtu mwingine kabisa alikuwa amesimama pale pale, akivuta sigara yake taratibu.
Nilimtazama kwa muda, kisha sauti yake ikajirudia kichwani kwangu:
“Ukinikumbuka, utanikumbuka kwa lipi?”
Nilitoa simu mfukoni. Nikampigia mama.
“Mama...”
“Abee mwanangu, salama?”
“Nakupenda sana.”
Kukawa na ukimya kidogo, kisha akajibu kwa sauti ya tabasamu:
“Na mimi nakupenda mwanangu.”
Nilikata simu. Sikujua kama kesho nitakuwa hai au la, lakini nilijua kitu kimoja: Leo bado nina nafasi.
Nafasi ya kupenda.
Nafasi ya kusema samahani.
Nafasi ya kutunza afya yangu.
Nafasi ya kuwatembelea watu wangu.
Nafasi ya kuanza kuchukua hatua.
Tangu siku hiyo, niliacha kuishi kama mtu aliye na uhakika na kesho. Maana nilishawahi kumpenda mtu aliyekuwa na mipango elfu moja ya kesho... lakini kesho yake haikuwahi kufika.