KUSALITIWA, KICHOCHEO CHA MAENDELEO YANGU
Jerome Nduwayo
August 27, 2026
5 min read
173 views
0 favorites
Open Access
Kijana mwanafunzi Jack baada ya kuumizwa na mapenzi aliamua kuwekeza nguvu kwenye kazi yake ya kutoa ushauri. Katika hali asiyoitarajia mmoja wa wateja wake alikuwa Alice mpenzi wake wa zamani aliyekuwa anahitaji huduma ya Jack kwa kiwango kikubwa sana. Je, Jack atachukua maamuzi gani dhidi ya Alice aliyemsababishia maumivu makali ya moyo?
Jack alikuwa kijana anayeishi mkoani Rumonge nchini Burundi. Alikuwa amefanya mtihani wa taifa wa darasa la kumi unaoruhusu kuendelea na darasa la kumi na moja. Alipokuwa anafanya kazi ndogondogo za nyumbani Baba yake aliyekuwa anasikiliza taarifa ya habari alimpa habari kuwa amefaulu vizuri na alama zake zinamruhusu kusoma shule za bweni. Jack alifurahi sana ila angelijua tukio ambalo lilikuwa linamsubiri huenda angelighairisha kwenda kwenye shule hiyo.
Siku ilifika akaenda kwenye shule ya sekondari ya Tora iliyopo mkoani Bururi. Alipofika bwenini mazingira ya hapo hayakuwa rahisi hususani baridi, chakula na kasi ya kula. Licha ya hayo, bahati ilikuwa kwake maana alijuana na Jimmy aliyekuwa anaisha mkoani Rumonge pia na kuwa mwenyeji wake.
Jack, mbali na kufanya vizuri darasani alikuwa pia mwanariadha mzuri na hilo lilimpatia umaarufu shuleni na kuwa gumzo kubwa kwenye bweni za wasichana wakitamani awe mpenzi wao. Kwa kuwa kipaumbele chake kilikuwa kusoma na kufaulu vizuri na kuendelea na chuo kikuu, maswala ya mahusiano hakuyatilia maanani.
Waliosema kuwa ‘Simba jike na ukali wote anazaa’ walikuwa sahihi maana msimamo wa Jack ulibadilika ghafla baadha ya kuona msichana mrembo Alice aliyehamia kwenye shule hiyo, pia katika darasa la kina Jack.
Alikuwa na muonekano wa sura nzuri isiyo na kipele. Kungelitokea mgonjwa mwenye kutibiwa na kipele cha usoni mwa Alice basi mgonjwa huyo angelistahili salamu ya buriani kwani asingelipona.
Alice hakuwa anapenda kujiremba kwa sababu urembo wake ulikuwa wa asili. Midomo yake haikuhitaji kuwekwa mafuta ya midomo ili ionekane vizuri. Alikuwa na matako makubwa kiasi cha kusingiziwa kuwa alifanyisha upasuaji ila haikuwa kweli. Kwa urembo wake, wahenga wangelipata muda wa kumwona waliposema hakuna kibaya kisicho na kasoro basi wangelirekebisha na kuongeza isipokuwa Alice tu.
Jack aliaanza kujenga mazoea na Alice hatimaye wakawa kwenye mahusiano ya kimapenzi. Walipeana ahadi nyingi kama kufunga ndoa, wakapanga idadi ya watoto watakaozaa, majina yao pamoja na malezi watakayowapatia.
Masomo yaliendelea, Jack na Alice wakahitimu wakiwa na ahadi za kutembeleana maana Alice alikuwa anaishi mjini Bujumbura unaopakana na mkoa wa Rumonge nyumbani kwa kina Jack.
Jioni moja, Jack akiwa yupo chumbani akiwa anazubaa mtandaoni alirushiwa picha na rafiki yake Jimmy kupitia "whatsapp" ikiwa imeambatanishwa na "emoji" za mshangao. Jioni hiyo ilikuwa mbaya kwa Jack kiasi cha kumfanya ajute kwa nini alizaliwa. Uchungu alioupata hakuwa amewahi kuuhisi.
Picha alipoifungua alishituka kuona ni mwaliko wa harusi. Harakaharaka aliangalia majina ya watu hao akashangaa kuona majina yote ya Alice mpenzi wake. Angelijiliwaza kuwa majina yanaweza kufanana ila alipata uhakika baada ya kuona picha ya Alice akiwa na mvulana mwingine.
Kijana huyo aliwatupia lawama waundaji wa Akili Bandia yaani Artificial Intelligence (AI) kwa kumshituwa maana hakuamini kuwa ni uhalisia. Kuthibitisha hilo alimpigia simu Alice.
Maneno aliyomwambia yalimvuruga sana maana hakuamini kuwa mtu aliyewahi kumpenda na kumpa ahadi nyingi za kutoachana na kutosababishiana maumivu anaweza kubadilisha mtazamo na ikawa kama vile hajawahi kumjua. Miongoni mwa maneno yaliyomuumiza sana Jack na kuzunguka kichwani mwake ni pale Alice alipomwambia hivi ‘Sikuwa nimekupenda kwa dhati ila nilitaka kuwa na wewe kwa sababu ya umaarufu wako ili wavulana wengine wasinisumbue kwa kujua kuwa tunapendana.’
Jack aliumia sana ila baada ya miezi kama mitatu kwa kujitafakari kwa kina na kwa msaada wa ushauri wa rafiki yake Jimmy aliamua kutokubali maumivu ya mapenzi yamuongoze na kumharibia maisha yake bali aliamua kuyatumia kuwa bora zaidi.
Kwa kuwa baada ya kuhitimu walikuwa wamefanya mtihani wa taifa wa kujiunga na chuo kikuu, matokeo yalipotoka Jack alikuwa amaefaulu na kuwa miongoni mwa wanaoweza kuendelea na masomo ya chuo kikuu cha Burundi na kikubwa zaidi alipewa idara aliyokuwa anaitaka ya Saikolojia bewani Kamenge mjini Bujumbura.
Alianza chuo na akapenda kusoma sana vitabu vinavyohusu saikolojia ya aina yoyote ile iwe ya binadamu, ya elimu, ya pesa, ya watoto, ya wanawake, ya wanaume,... Kando ya kusoma vitabu alikuwa anapenda kuhudhuria semina mbalimbali zinazohusu uchumba na ndoa zilizokuwa zinatokea mjini Bujumbura au kwenye mitandao ya kijamii.
Alipomaliza chuo alifungua kampuni yake ya kutoa mafunzo na ushauri kuhusu mahusiano ya kimapenzi, uchumba na ndoa ili kusaidia vijana na watu wazima wanaoteswa na mapenzi na kuwafanya wapatwe na msongo wa mawazo na kupoteza tumaini la maisha.
Siku moja akiwa ofisini alipokea simu ya mama mmoja akiwa analia kwa kwikwi kuwa anahitaji msaada wake. Jack alimwelekeza ofisi yake ilipo na mwana mama huyo akafika. Jack alipomwona alipigwa na butwaa kwa jinsi alivyokuwa amekonda pamoja na kupauka usoni. Kwa kuwa Jack alikuwa amenenepa na kunawiri, mteja huyo hakumjua ila Jack alimkumbuka vizuri mteja wake lakini Jack alikaa kimya ili kwanza afanye kazi maana alijua kwamba mteja wake angelijua kuwa huyo ndiye Jack basi angelikosa uhuru na ujasiri wa kumweleza shida yake.
Mteja huyo alimsimulia Jack jinsi mume wake anavyomnyanyasa kwa kumpiga na kuleta wanawake nyumbani na kuzini nao akishuhudia. Jack alimsikiliza kwa makini na kumwuliza jinsi hali hiyo ilivyoanza na jinsi ilivyoendelea. Kwa utaalamu na tajiriba yake hilo lilikuwa tatizo dogo sana kama kuweka dole gumba "like" kwenye chapisho la "Facebook". Alimpa ushauri mteja wake wa jinsi ya kubadilisha tabia yake na mambo ya kufanya kipindi mumewe anapoleta wanawake. Mbinu alizompatia zilimsaidia mteja wake na kumfanya mume wake kurudi kuwa mume bora kama wa zamani. Mteja huyo alinawiri na kurudi kuwa na mwili wake wa zamani kisha akataka kumshukuru mwanasaikolojia aliyemsaidia kurudisha amani kwenye ndoa yake.
Baada ya kukaa mahali walipokutania mteja wa Jack alimwangalia sana Jack kama vile anamfananisha na mtu aliyewahi kumwona na kweli aligundua kuwa ni Jack mpenzi wake wa zamani.
Papohapo alipiga magoti chini akilia na kusema:
''Jack naomba unisamehe sana. Nilikutenda kwa kufunga ndoa na mwanaume mwingine kwa tamaa ya pesa ila ona wewe ndiwe uliyekomboa furaha yangu. Ulivyo na moyo wa tofauti umenisaidia ukiwa umenijua na kukumbuka mabaya niliyokufanyia.’’
Jack alimnyanyua na kumwambia: ‘Usijali Alice. Nilishakusamehe zamani. Kila jambo linatokea kwa mpamgo wa Mungu. Ninakushukuru pia mimi kwa yale uliyoyafanya kwa kuwa usingelifanya yale nisingelipata kichocheo cha kufika hapa nilipo. Maumivu uliyonisababishia niliyatumia vizuri na kuweza kuyazalisha matunda na hivi sasa ni mshauri bora nchini na nje ya nchi kwa kutatua matatizo ya mahusiano, uchumba na ndoa.’ Baada ya hapo walikumbatiana na kuendelea kupiga stori za hapa na pale.