EastAfricaIsWriting

Stories That Speak in Many Tongues

  • Home
  • Browse
  • About
  • Contact
  • Login
  • Join as Writer
  • Donate

Quick Links

  • About Us
  • Author Guidelines
  • Contact

Categories

  • Football Review
  • Articles
  • Creative Essays
  • Stories
  • Fiction

Connect

© 2026 EastAfricaIsWriting. All rights reserved.

  • Privacy Policy
  • Terms of Service

TUNAONGEA ZAIDI, LAKINI JE, TUNAWASILIANA VIZURI?

GASPAL LUCAS JEREMIA
Articles
August 27, 2026
4 min read
176 views
0 favorites
Open Access

“Tunaongea Zaidi, Lakini Je, Tunawasiliana Vizuri?” ni makala inayochunguza namna teknolojia na mitandao ya kijamii ilivyobadilisha mawasiliano miongoni mwa vijana. Makala hii inaangazia pande chanya na hasi za mabadiliko hayo, ikionyesha jinsi mawasiliano ya kidijitali yanavyoweza kuwapa vijana maarifa, watu wa kuwajenga na fursa mpya, lakini pia yanaweza kusababisha kutokuelewana, kuvunjana moyo na udhalilishaji wa hadharani. Makala inasisitiza umuhimu wa kufikiri kabla ya kuchapisha, kusikiliza kabla ya kujibu, kutatua masuala ya kibinafsi kwa heshima na kutumia nguvu ya mitandao kujenga badala ya kubomoa. Hoja kuu ni kwamba teknolojia imetupa sauti, lakini heshima na uelewano bado ni jukumu letu wenyewe kuyajenga.

TUNAONGEA ZAIDI, LAKINI JE, TUNAWASILIANA VIZURI? Kwa kipindi hiki, teknolojia imetuletea njia nyingi zaidi za kuwasiliana kuliko enzi za mababu zetu. Tunaweza kuwasiliana na mtu yeyote, haijalishi yuko umbali gani, kwa sekunde chache kupitia simu na mitandao ya kijamii. Tunaweza kujifunza kutoka kwa watu wapya, kupata mawazo mapya na hata kujenga mahusiano na watu ambao tusingekuwa na nafasi ya kukutana nao katika maisha ya kawaida. Lakini pamoja na fursa zote hizi, kwa nini bado tunapata ugumu wa kuelewana? Mimi, kutokana na mazungumzo mengi ninayoyaona na kuyashuhudia miongoni mwa vijana, naweza kusema kuwa mabadiliko haya yanaonekana kwa pande mbili: chanya na hasi, kulingana na mazingira na watu tunaokutana nao Kwa upande chanya, mitandao imewawezesha vijana kukutana na watu wapya, kujifunza vitu vipya kutoka kwao na kupata watu wanaowatia moyo. Wengine huenda mbali zaidi kwa kuwashika mkono katika vitu wanavyovifanya, kuwafundisha na kuwapa nguvu katika wanachokifanya; jambo linaloweza kubadilisha namna wanavyofikiri na kuwasaidia kukua. Lakini upande wa hasi, si kila mtu wanayekutana naye mtandaoni anawaletea nguvu. Wengine huwavunja moyo, wengine hudharau kile wanachofanya, na maneno au matendo hayo yanaweza kuathiri namna vijana wanavyojiona na maamuzi wanayofanya. Hivyo, mawasiliano yanaweza kuwa nguvu ya kujenga au kuvunja mtu, kutegemea aina ya watu na maudhui wanayokutana nayo. Hali hii kwa kiasi kikubwa inatokana na hofu inayoweza kujitokeza tunapokutana na wahusika ana kwa ana. Wengi wetu tunapokuwa mtandaoni tunaonekana kuwa wazungumzaji wazuri na wenye ujasiri, kwa sababu hatuko moja kwa moja mbele ya mtu tunayemzungumzia. Tunapata nafasi ya kuandika, kufikiria na kuchagua maneno yetu bila kukutana mara moja na hisia au majibu ya mtu mwingine. Wakati mwingine tunasema mambo makubwa mtandaoni kwa sababu tunayozungumzia hayamlengi mtu moja kwa moja, lakini tunapokutana na mhusika ana kwa ana, ujasiri huo unaweza kupungua. Hapa ndipo tunapaswa kujiuliza: je, tunajenga uwezo wa kuwasiliana, au tunajenga uwezo wa kuongea pale ambapo hatulazimiki kukabiliana na majibu? Tatizo huwa kubwa zaidi pale mawasiliano yanapotumika kumdhalilisha mtu mbele ya hadhira. Jambo ambalo zamani lingeweza kubaki kati ya watu wawili sasa linaweza kuhamishwa kwenye WhatsApp Status, Instagram au TikTok na kuonekana na watu wengi kwa muda mfupi. Picha, video, maneno ya kejeli au ujumbe unaomlenga mtu vinaweza kusababisha aibu ambayo si ya mtu mmoja tena, bali inakuwa tukio linaloshuhudiwa na marafiki, ndugu, wanafunzi au wafanyakazi wenzake. Wakati mwingine watu wengine huongeza vicheko, maoni au kusambaza maudhui hayo, na hivyo kuongeza ukubwa wa tatizo. Hapo mawasiliano yanapoteza kusudi lake la kujenga uelewano na kugeuka kuwa chombo cha kumvunjia mwingine heshima. Madhara ya udhalilishaji wa aina hii yanaweza kuwa makubwa zaidi kwa sababu maudhui ya kidijitali yanaweza kuhifadhiwa, kupigwa screenshot, kupakuliwa na kusambazwa tena hata baada ya mtu kujaribu kuyaondoa. Kwa kijana aliyedhalilishwa, jambo hilo linaweza kuathiri namna anavyojiona, uhusiano wake na wengine na hata ujasiri wa kushiriki katika mazingira ya kijamii. Hii ndiyo sababu tunapaswa kujiuliza kabla ya kuchapisha jambo linalomhusu mwingine: Je, tunatumia uhuru wetu wa kusema kujenga mazungumzo, au tunatumia hadhira tuliyopewa kumuumiza mtu? Kama tunataka mawasiliano ya kidijitali yawe sehemu ya kujenga jamii bora, vijana wanapaswa kuanza na jambo rahisi: kufikiria kabla ya kuchapisha. Kabla ya kuweka status, kuandika comment au kushiriki maudhui yanayomhusu mtu mwingine, ni muhimu kujiuliza kama tungependa kuambiwa jambo hilo kwa namna hiyo mbele ya watu. Ikiwa tuna tatizo na mtu, si lazima kila jambo lipelekwe hadharani; mazungumzo ya faragha, ujumbe binafsi au mazungumzo ya ana kwa ana yanaweza kutoa nafasi ya kuelewana bila kuongeza aibu na chuki. Pia, tunapaswa kuwa tayari kusimama na mtu anayelengwa na udhalilishaji badala ya kucheka, kushiriki au kuongeza nguvu kwenye maudhui yanayomuumiza. Ushawishi tulio nao mtandaoni ni chombo; tunaweza kuutumia kujenga, kutia moyo na kutambua mema ya wengine, au kuutumia kuwavunja. Chaguo hilo liko mikononi mwetu. Tunaongea zaidi, lakini je, tunawasiliana vizuri? Tumeshapata uwezo wa kusema kila kijana leo ana jukwaa, ana sauti, ana likes na followers. Lakini kuwa na sauti nyingi na uwezo mkubwa wa kusema si sawa na kuwa na uwezo wa kuelewana. Sasa tunahitaji kujifunza kuelewana: kusikiliza kabla ya kujibu, kutafakari kabla ya kuchapisha na kutambua kwamba nyuma ya kila akaunti kuna mtu mwenye hisia halisi. Ujasiri wa kweli si ule wa kuandika maneno makali nyuma ya screen ambako hakuna anayekuona machoni. Ujasiri wa kweli ni ule wa kuzungumza kwa heshima, kusikiliza kwa makini, kukubali kwamba mtu mwingine anaweza kufikiri tofauti na wewe, na kukabiliana na mtu ana kwa ana pale mgogoro unapohitaji hilo badala ya kukimbilia kuandika status au comment. Kama ningeweza kuacha ujumbe mmoja tu, ungekuwa huu: Teknolojia imetupa sauti, lakini heshima na uelewano bado ni jukumu letu wenyewe kuyajenga. Simu haiwezi kukufundisha kusikiliza, na likes haziwezi kupima kama umeeleweka kweli. Kadiri unavyokuwa na uwezo mkubwa wa kusema, ndivyo unavyohitaji hekima kubwa zaidi ya kujua ni lini ukae kimya, ni lini uzungumze faragha na ni lini uwe sauti inayojenga badala ya kubomoa.
Login to Favorite

About the Author

G

GASPAL LUCAS JEREMIA

@GASPAL

Helping people shift their mindset & build a life of value. Leadership | Business | Personal Growth Turning Vision Into Value. am I game changer

You May Also Like

BASIC NEED

Deo Moshi 2 min

Umuhimu wa hitaji la upendo kwenye jamii na dunia yetu

Usisikilize Kila Anachosema Mtu za kuambiwa changanya na zako

Thomas A. Kauky 2 min

Baba mmoja alifanya safari kwa kutumia farasi akisafiri na mwanae akiwa amempandisha mtoto juu ya fa...

LOVE AS HIGHEST FORCE

Thomas A. Kauky 5 min

What if the strongest force in the world is something we cannot see? A simple question asked by ...

TUPO KIZAZI KINACHOONGEA LAKINI HAKISIKILIZANI NA KUELEWANA.

Daudi Abel James 4 min

Kwa kifupi, mawasiliano ndio kiungo na daraja pekee la kuwaunganisha watu kwenye maisha ya kila siku...