Usisikilize Kila Anachosema Mtu za kuambiwa changanya na zako
Thomas A. Kauky
August 27, 2026
2 min read
153 views
1 favorites
Open Access
Baba mmoja alifanya safari kwa kutumia farasi akisafiri na mwanae akiwa amempandisha mtoto juu ya farasi. Sasa, watu walipomuona wakasema,
“Huyu mtoto hana adabu kabisa! Yaani baba yake ndiye ana...
Baba mmoja alifanya safari kwa kutumia farasi akisafiri na mwanae akiwa amempandisha mtoto juu ya farasi. Sasa, watu walipomuona wakasema,
“Huyu mtoto hana adabu kabisa! Yaani baba yake ndiye anatembea kwa miguu, badala yake yeye amempandishe baba yake?”
Mtoto akaona isiwe kesi, akamwambia baba yake apande juu ya farasi. Wakaenda mbele kidogo, watu wakawaona na kusema,
“Huyu baba ana huruma kweli! Inawezekanaje mtoto anamwendesha farasi, ingali yeye ni mkubwa na anaweza kutembea umbali mrefu?” Baba akaona isiwe kesi pia, wakaamua wapande wote juu ya farasi.
Guess what? Watu wengine wakawaona na kusema,
“Hivi hawa binadamu mbona ni wakatili kiasi hiki? Yaani wanamnyanyasa huyu farasi kiasi hiki?” Kwa sababu baba na mtoto walikuwa wanawasikiliza watu, wakaamua kushuka kutoka kwenye farasi. Mwisho wa safari, wakafika wakiwa wamembeba yule farasi! Ungewaona, na wewe si ungesema, “Ona hawa wehu!” 😂
Vivyo hivyo kwenye maisha yetu, tukiendelea kusikiliza watu sana pale wanapotukatisha tamaa au kututoa nje ya reli tutafika mwisho tukiwa kama wehu, tukiwa tumeubeba farasi badala ya farasi kutubeba.
Unajua tunachopaswa kufanya? Weka pamba masikioni! Kama kitu unachokiamini ni sahihi na hakimuumizi mwingine, kuwa na uthubutu wa kukifanya. Fanya, mtu wangu! Watu watasema tu. Ufanye mazuri watasema, ufanye mabaya watasema; hata usipofanya chochote, bado watasema. Ndivyo tulivyo sisi wana wa Adamu.
Usipoteze furaha yako kwa kuwafanya wengine wafurahi....... Ukihisi unaweza kumfurahisha kila mtu, kumbuka huwezi.
Jitahidi kulinda furaha yako na kuishi maisha yako kwa hekima, bila kuruhusu kila maoni ya mtu yakuelekeze. Maana ukijaribu kumridhisha kila mtu, mwisho wa siku utajikuta umebeba farasi mgongoni.