TUPO KIZAZI KINACHOONGEA LAKINI HAKISIKILIZANI NA KUELEWANA.
Daudi Abel James
August 27, 2026
4 min read
157 views
0 favorites
Open Access
Kwa kifupi, mawasiliano ndio kiungo na daraja pekee la kuwaunganisha watu kwenye maisha ya kila siku.
Iwe kwenye kazi, biashara, Siasa, uongozi na maeneo mengine muhimu ya maisha yetu.
Wazungu wakasema "If there is no communication there is no relationship" yaani (kama hakuna mawasiliano basi hakuna mahusiano).
Tudumishe mbinu za mawasiliano kuendana na nyakati tulizopo leo.
Tuiishie kuambiana au kuongea ila tukashindwa kusikilizana na kuelewana.
Ahsante!.

Tupo Kizazi Kinachoongea Lakini Hakisikilizani na Kuelewana.
Mapinduzi ya Teknolojia Yamekuja Lakini Yamepoteza Mawasiliano ya Kweli.
Dunia ya leo imefanya mawasiliano kuwa rahisi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu.
Kwa sekunde chache tunaweza kuzungumza na mtu aliye popote duniani, kwa kutuma ujumbe, kushirikina kwa mawazo na kuunganisha watu kupitia teknolojia.
Lakini pamoja na maendeleo haya makubwa, tunapaswa kujiuliza. Je, tumekuwa na uwezo mkubwa wa kuwasiliana au tumepoteza uwezo wa kusikilizana na kuelewana?.
Ukweli ni kwamba kizazi cha sasa kina njia nyingi za kuwasiliana, lakini kinaonekana kupoteza jambo muhimu zaidi mawasiliano yenye maana.
Leo tunaweza kuwa na maelfu ya marafiki kwenye mitandao ya kijamii, lakini bado watu wengi wanajisikia wapweke, hawasikilizwi na hawaeleweki.
Tatizo la dunia ya sasa si ukosefu wa mawasiliano. Tatizo ni kupotea kwa sanaa ya kusikilizana na kuelewana. Hatukatai kwamba teknolojia imeleta mapinduzi makubwa katika maisha yetu.
Imeturahisishia kupata taarifa, kufanya biashara, kujifunza na kuendelea kuwa karibu na watu walioko mbali. Lakini mabadiliko haya yamekuja na changamoto yake.
Zamani, mawasiliano yalihitaji ukaribu wa mtu na mtu. Watu walikaa pamoja, walitazamana machoni na waliweza kuelewana na kusikilizana (kuwasiliana) kupitia sauti, hisia na matendo.
Leo, mawasiliano mengi yamekuwa ya haraka. Ujumbe mfupi, emoji na majibu ya sekunde chache vimechukua nafasi ya mazungumzo marefu yenye kina.
Tumeboresha kasi ya kuwasiliana, lakini tumepunguza ukaribu wa mtu na mtu. Mtu anaweza kuwa online muda wote lakini asiwepo kihisia na watu wanaomzunguka.
Anaweza kuwa na followers wengi lakini akakosa mtu wa kuzungumza naye kwa undani. Hii inatufundisha kwamba uwepo wa kidijitali hauwezi kuchukua nafasi ya uwepo wa kihisia.
Changamoto kubwa ya mawasiliano ya leo si watu kushindwa kuongea, bali ni watu kushindwa kusikilizana na kuelewana. Wengi hawasikilizi ili kuelewa, bali wanasikiliza ili kujibu.
Katika mahusiano, familia na jamii, kila mtu anataka kusikika, lakini wachache wako tayari kutoa nafasi ya kumsikiliza mwingine.
Kusikiliza si kukaa kimya wakati mtu mwingine anazungumza.
Kusikiliza ni kuelewa hisia, kuheshimu mtazamo wa mwingine na kujaribu kuona jambo kupitia macho yake.
Jamii yenye watu wanaojua kusikiliza ni jamii yenye uwezo mkubwa wa kujenga mahusiano yenye afya. Moja ya mabadiliko makubwa yaliyokuja na mitandao ya kijamii ni namna watu wanavyotafuta kuthibitishwa (Validation).
Watu wengi wameanza kupima thamani yao kupitia likes, comments na idadi ya wanaowafuata.
Lakini kuna tofauti kubwa kati ya attention na connection. Attention ni pale watu wanakuona. Connection ni pale mtu anakuelewa.
Mtu anaweza kupata sifa kutoka kwa maelfu ya watu lakini akawa hana mtu anayemjua kwa undani. Anaweza kuonyesha furaha mtandaoni lakini ndani yake akawa anapambana na changamoto ambazo hakuna anayeziona.
Tumekuwa kizazi kinachojua kuonyesha maisha yetu, lakini wakati mwingine tunasahau kuishi na kujenga mahusiano ya kweli.
Mabadiliko haya yameathiri sana mahusiano ya kimapenzi na kijamii. Watu wengi wamejifunza kuanzisha mahusiano kupitia ujumbe wa simu, lakini wanashindwa pale wanapohitaji mazungumzo ya kina.
Mahusiano hayajengwi na maneno matamu pekee. Yanajengwa na uwezo wa kuzungumza kuhusu hofu, matarajio, maumivu na changamoto.
Changamoto ya kizazi hiki ni kwamba watu wengi wanapenda mawasiliano mepesi, lakini wanakwepa mazungumzo magumu.
Wanataka kueleweka, lakini hawajifunzi kuelewa. Wanataka kupendwa, lakini hawajifunzi kueleza namna wanavyohitaji kupendwa.
Mawasiliano yasiyo na kina yanaweza kuwafanya watu wawili wakae pamoja lakini wawe mbali kihisia.
Suluhisho si kuikataa teknolojia.
Teknolojia si tatizo, tatizo ni namna tunavyoitumia.
Tunapaswa kujifunza kuunganisha maendeleo ya kisasa na misingi ya kibinadamu.
Tunahitaji kurudisha mazungumzo ya ana kwa ana, kwa sababu kuna hisia ambazo haziwezi kuelezwa kupitia simu au mtandao.
Tunahitaji kujifunza kusikiliza kwa moyo, kwa sababu wakati mwingine mtu hahitaji ushauri bali anahitaji kuhisi kuwa anaeleweka.
Pia tunahitaji kuwa wa kweli zaidi. Dunia haihitaji watu wanaoonyesha maisha yasiyo na changamoto, bali inahitaji watu wanaoweza kuwa waaminifu kuhusu safari zao.
Mawasiliano si uwezo wa kuongea tu. Ni uwezo wa kujenga maelewano kati ya mioyo miwili.
Mwisho...
Kizazi chetu kina nafasi kubwa ya kutumia teknolojia kujenga dunia bora. Tuna uwezo wa kuunganisha watu wengi kuliko kizazi chochote kilichopita.
Lakini hatupaswi kusahau jambo moja muhimu, Mwanadamu hahitaji tu ujumbe mwingi; anahitaji kueleweka.
Hahitaji tu watu wanaomfuata; anahitaji watu wanaomjali. Hahitaji tu mawasiliano mengi; anahitaji mawasiliano yenye maana.
Tukisimama kwenye mawasiliano ya kusikilizana na kuelewana basi mahusiano, kazi, biashara na kila kitu kitaenda vyema sana.
Written By Magille
About the Author
D
Daudi Abel James
@Daudi04
Relationship and Marriage, Author and Public Speaker